Baada ya kusubili kwa miaka 38 ya kufuzu kushiriki kombe la Mataifa ya Africa (AFCON), hatimaye yametimia kwa timu ya taifa ya Uganda kumaliza ukame huo wa kusubili miaka yote hiyo baada ya hapo jana kuifunga goli 1-0 timu ya taifa ya Comoro mbele ya mashabiki waliojazana kuishuhudia timu hiyo kwenye uwanja wa Nelson Mandela nchini Uganda. Ni mchezaji Farouk Miya alieshinda goli pekee na la ushindi kwa taifa lake.
The Cranes wamefanikiwa kufuzu wakiwa wapili nyuma ya Burkina Faso kwenye kundi lao lililokuwa linaonekana gumu, huku vinara wa kundi hilo Burkina Faso wao wakiifunga Botswana goli 2-1.
Wakiwa na pointi zao 13 baada ya mechi zote, Uganda wamemaliza hatua hiyo iliyowafanya kuonekana bora dhidi ya kundi D lililokuwa linaonekana gumu kwao. Walijitahidi kupambana kupata ushindi dhidi ya wageni hao ambao walikuwa imara kipindi cha kwanza cha mchezo, Uganda walipata kona nne ndani ya dakika 15 za mwanzo.
Shukrani zaidi zilienda kwa golkipa wa Comoro Ali Ahamada ambae alifanya kazi ya ziada kuondoa hatari nyingi zilizolengwa golini kwake kutoka upande pinzani, lakini bahati haikuwa yao pale Farouk Miya alipowanyanyua vitini mashabiki uwanjani kwa goli lake la dakika 35 ya mchezo kabla ya mapumziko goli lililodumu mpaka mwisho wa mchezo huo hapo jana.
Timu zilizofuzu ni pamoja na Mali, Jamhuri ya Congo, Tunisia, Burkina Faso, Guinea Bissau, Morocco, Misri, Ghana, Ivory Coast, Algeria, Senegal, Zimbambwe, Cameroon, Uganda, Togo, na wenyeji Gabon. Na tarehe 19 Oktoba itafanyika droo ya upangaji makundi kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajia kuanza tarehe 14 Januari 2017 mpaka tarehe 5 Februari 2017 nchini Gabon.

No comments:
Post a Comment