Sunday, October 9, 2016

ASHANTI YAJIGAMBA DHIDI YA FRIENDS RANGERS LIGI DARAJA LA KWANZA.


Leo kuna mechi za Ligi Daraja la Kwanza zinazotarajiwa kuendelea leo kwenye viwanja vitano tofauti, kocha wa Ashanti United Maalim Swaleh amejigamba kuisambaratisha Friends Rangers kwenye mchezo utakaochezwa Uwanja wa Karume, Ilala Dar es Salaam.


Akizungumza na gazeti hili jana kocha Swaleh alisema ushindi ni muhimu ili kujiweka pazuri kwani ligi ya safari hii ina ushindani mkubwa.
“Nimewaandaa wachezaji wangu kimbinu na kisaikolojia ili tuhakikishe tunashinda mchezo huu kwani una ushindani na naamini tuna uwezo wa kushinda mchezo huu japo Friends Rangers siyo timu ya kubeza,” alisema Swaleh.
Ashanti United imeshacheza michezo miwili na kushinda yote inaonekana kupania kurudi Ligi Kuu msimu ujao japo timu hiyo haina kiungo namba sita jambo linalosababisha kushambuliwa mara nyingi.
Mechi ya Ashanti na Friends huwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote kuwa na mashabiki wengi wa soka, Ashanti ikikusanya mashabiki wa Ilala na Friends ikiwa na mashabiki kutoka Manzese na Magomeni.
Katika kundi B, JKT Mlale itacheza na Polisi Moro kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Njombe Mji itaikaribisha Kemondo wakati KMC itacheza na Mbeya Warriors kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Nalo kundi C Rhino ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Mgambo JKT ya Tanga na kesho Mshikamano ya Dar es Salaam itacheza na Lipuli ya Iringa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment