Kikosi cha Toto Africans. |
Klabu ya Toto Africans ya Mwanza hapo juzi walikuwa na mkutano wa dharula wa wanachama wa klabu hiyo na kupitia mkutano huo uongozi wa klabu hiyo umewasimamisha baadhi ya viongozi wake kutokana na utovu wa nidhamu.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godwin Aiko alisema sababu kubwa ya kuwasimamisha viongozi hao ni kutokana na utovu wa nidhamu na kutokumheshimu yeye kama mwenyekiti.
Viongozi waliosimamishwa ni Isack Mwanahapa na Saleh Akida ambao ni wajumbe wa kamati ya Utendaji ya klabu hiyo. Aiko alisema wanachama waliosimamishwa Mei mwaka huu wamesamehewa rasmi na wameruhusiwa kuendelea na shughuli za klabu.
Wanachama waliosamehewa ni Beatus Madenge, John Kisura na Kipalata Ngassa. Wanachama hao walikumbwa na adhabu ya kusimamishwa baada ya kusababisha vurugu katika mechi ya Toto dhidi ya Yanga iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Siku ya tukio wanachama hao walivamia gari la katibu wao Ernest Mpio kugombea fedha za mapato ya mechi hiyo wakitaka walipwe posho ndipo gari liondoke.
“Kuhusu suala la makamu mwenyekiti Ahmed Gao ambae pia alisimamishwa bado tunalifanyia kazi,” alisema. Gao alisimamishwa kutokana na kosa la kujitangaza hadharani kuwa avuliwe uongozi kwa muda kwa sababu ya mechi ya Yanga na kutangaza hadharani kwamba yeye ni mwanachama wa Yanga kwa moyo wake wote.
Hatua ya Toto kuwasimamisha viongozi hao imekuja siku chache baada ya kujiuzulu kwa kocha Rogasian Kaijage aliyeanza kufundisha timu hiyo mwanzoni mwa msimu akichukua mikoba ya John Tegete.
Kocha Kaijage aliamua kubwaga manyanga baada ya kuonekana kutokubalika kwa mashabiki wa timu hiyo, huku mwenyewe akidai wamekuwa wakimuingilia kwenye majukumu yake. Mikoba ya Toto sasa iko chini ya kocha Halfani Ngassa.
No comments:
Post a Comment