Tuesday, September 6, 2016

AIRTEL RISING STARS KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO


Mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa yanatarajiwa kuanza leo jumanne, Septemba 6, 2016 katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es salaam. Huku timu za soka za wasichana za Lindi na Arusha zimepangwa kukutana katika mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo.

Mashindano hayo yatafunguliwa rasmi siku ya leo mchana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mheshimiwa Paul Makonda ambaye atashuhudia mechi ngumu ya wavulana kati ya Mwanza na Ilala. Mashindano hayo yanayojumuisha timu za wasichana na wavulana  yenye lengo la kuibua vipaji nchini yatajumuisha timu nyingine za Mbeya, Temeke, Lindi, Kinondoni,  Arusha, Zanzibar na Morogoro. Tayari timu zimeshawasili na ziko kambini katika shule ya Filbert Bay iliyopo Kibaha. 


  
                                          Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde akiongea wakati wa kuchezesha droo ya upangaji makundi  wa michuano hiyo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars, katikati ni Mkurugenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi na kushoto yake ni  Mkurugenzi wa maendeleo ya soka la wanawake TFF Amina Karuma.
 
 Ofisa huyo Uhusiano w Airtel Tanzania bi Jane Matinde, alisema kuwa kampuni yake inajivunia kuweza kutoa mchango katika soka la Tanzania, '' Airtel Rising Stars imekuwa chanzo cha kutumainiwa kwa klabu na timu za Taifa kwa kupata vijana chipukizi wenye vipaji. Tunaona fahari kuweza kupata fursa ya kudhamini soka nchini Tanzania''.

Pia akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kupanga makundi hapo jana iliyofanyika katika ofisi za shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Mkurugenzi wa Ufundi Mwalimu Salum Madadi alisema kuwa maandalizi yote ya mashindano hayo ngazi ya taifa yamekamilika. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa maendeleo ya soka la wanawake nchini Bi Amina Karuma ambaye aliyaelezea mashindano hayo kuwa ni chemchem ya wanasoka chipukizi kwa wasichana na wavulana.

'' Mashindano haya yametusaidia kupata wachezaji wenye vipaji vya ajabu ambao wanaunda timu za Serengeti Boys na timu ya taifa ya wanawake yani Twigwa Stars na kuwashukuru Airtel Tanzania kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo''.

Michuano hii ya Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa inatarajia kufika tamati siku ya jumapili,september 11, 2016. ambapo mabingwa wa pande zote mbili kwa wasichana na wavulana watapatikana na kukabidhiwa vikombe vya ubingwa. Na vilevile TFF itatangaza wachezaji nyota kwa wasichana na wavulana wataochaguliwa kuunda timu ya Airtel Rising Stars kwa mwaka huu 2016.






No comments:

Post a Comment