Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Azam na Simba ya Dar es salaam, utafanyika jumatano Septemba 21,2016 badala ya Septemba 17 mwaka huu.
Mchezo huo utakaofanyika uwanja wa Taifa, umesogezwa mbele kuipisha timu ya Taifa ya Congo-Brazzaville ipate nafasi ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Taifa, ikiwa ni kutekeleza matakwa ya kanuni za michezo wa mpira wa miguu za kimataifa kwamba mwenyeji lazima aachie uwanja kwa siku moja au masaa 24 kabla ya mchezo wa ushindani.
Congo-Brazzaville watakuwa wageni nchini kucheza na Serengeti Boys ambayo ni timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Mchezo huo utafanyika Septemba 18,2016 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Serengeti Boys kwa sasa iko Shelisheli ikijiandaa na mchezo huo ambako imejipanga vyema kuiondoa Congo-Brazzaville katika michezo miwili inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali ukianzia huo wa Septemba 18,2016 kabla ya kurudiana jijini Brazzaville hapo ama Septemba 30, au Oktoba 1 au Oktoba 2, mwaka huu.
Chanzo - TFF

No comments:
Post a Comment