Friday, October 14, 2016

KALLY AJIPA MOYO MAJIMAJI.

Kally Ongara kocha wa Majimaji.
Licha ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar 1-0 kwenye uwanja wa nyumbani, kocha wa Majimaji Kalimangonga Ongalla amesema kupoteza mchezo huo ilikuwa bahati mbaya na kwamba watarekebisha makosa yao kwenye mechi zijazo.

Timu hiyo inayoshika mkia inatarajia kucheza mchezo ujao dhidi ya Toto African utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza keshokutwa.

Kally alisema timu yake ilitawala mpira kwa asilimia kubwa katika mchezo huo lakini kwa bahati mbaya walijisahau na kufungwa bao hilo.

“Ukiangalia mchezo mzima, sisi tulicheza vizuri sema tulishindwa kutumia nafasi tulizopata katika kufunga, wenzetu walipata nafasi na kutufunga,” alisema.

Kally alisema wanaendelea kurekebisha penye makosa na taratibu mambo yatabadilika kwani kinachohitajika ni uvumilivu kwa mashabiki wa timu hiyo.

Majimaji msimu huu mambo yamekuwa mabaya baada ya kupoteza michezo minane kati ya tisa iliyocheza.

Tangu Kally ajiunge na timu hiyo amepoteza michezo miwili na kushinda moja, huku akijipa moyo kuwa mambo yatabadilika muda si mrefu.

Alisema lolote linawezekana kwani kuna michezo mingi iko mbele na kwamba wanaendelea na maandalizi kujiimarisha ili kupata matokeo mazuri.

No comments:

Post a Comment