![]() |
| Wachezaji wa Mamelodi Soundowns wakisherehekea ubingwa wao. |
Klabu ya Mamelodi Sundowns ya
Afrika Kusini imeshinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza
baada ya kuwalaza Zamalek wa Misri kwa jumla ya mabao 3-1 kwenye
fainali.
Kwenye mechi ya marudiano ya fainali mjini Alexandria,
Zamalek walipata ushindi wa 1-0 Jumapili lakini haukutosha kwani
walikuwa wamelazwa 3-0 na Sundowns mechi ya kwanza mjini Atteridgeville
Jumamosi wiki iliyopita.
Hii ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo ya Afrika Kusini kushinda kombe hilo.
Mara yao ya mwisho kufika fainali ilikuwa mwaka 2001 walipolazwa na mahasimu wakuu wa Zamalek, Al Ahly.
Zamalek walipata bao lao la pekee Jumapili dakika ya 62 kupitia Stanley Ohawuchi.
Kipa
wa Sundowns Denis Onyango aliumia kwenye goti dakika ya 12 na
akaondolewa uwanjani kwa machela dakika ya 28. Wayne Sandilands
alichukua nafasi yake.
Maafisa wa Misri, ambao awali walikuwa
wamesema ni mashabiki 20,000 pekee wangeruhusiwa uwanja wa Borg El Arab
kwa sababu za kiusalama walibadilisha msimamo wao na kuruhusu theluthi
tatu ya viti kwenye uwanja huo unaotoshea mashabiki 86,000 kujazwa.

No comments:
Post a Comment