![]() | |
| Mchezaji wa zamani wa Simba SC, ambaye sasa ni meneja wa klabu hiyo Musa Mgosi |
Simba ikiwa kinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa na pointi 20 huku ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja katika mechi zake nane zilizocheza msimu huu.
Meneja wa klabu ya Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema siri ya timu
yao kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni
ubora wa kikosi walichokisajili pamoja na umoja na mshikamano waliokuwa
nao.
Alizungumza hayo juzi baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi
ya Mbeya City Mgosi, mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, alisema ubora
waliokuwa nao msimu huu ni vigumu kuwazuia kwa sababu wamekamilika
katika idara zote muhimu ambazo ndizo zinachangia wapate matokeo hayo
mazuri.
“Ukweli wale wanaosubiri kuona tunapoteza watasubiri sana, Simba ya
msimu huu ina mabadiliko makubwa kuanzia wachezaji wote waliosajiliwa
unaweza kuona kila nafasi ina wachezaji watatu hadi wanne lakini hata
benchi la ufundi nalo ni bora kuanzia kocha mkuu hadi msaidizi wake
sioni sababu ya kushindwa kufanya vizuri,” alisema Mgosi.
Mkongwe huyo aliyestaafu soka mwanzoni mwa msimu huu na kukabidhiwa
cheo hicho cha Umeneja alisema, pamoja na kasi waliyoanza nayo lakini
mambo bado kwani malengo yao ni kuhakikisha wanaendelea na kasi hiyo na
kuhakikisha wanarudisha furaha kwa mashabiki wao wote wanaoipenda Simba
katika kipindi chote ambacho walikaa na majonzi kutokana na timu hiyo
kufanya vibaya.
“Dhamira yetu ni kwanza kuhakikisha tunashinda ubingwa wa Ligi Kuu,
ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa na pia kurudisha
furaha kwa kila shabiki na Mwanachama wa Simba ambaye alipoteza furaha
kipindi chote cha misimu mitatu ambacho timu ilikuwa haifanyi vizuri,”
alisema Mgosi.
Simba chini ya kocha Joseph Omog, imeshinda mechi sita na kutoka sare
mbili, matokeo ambayo yameonesha kuvunja rekodi ya timu hiyo kwa misimu
mitatu iliyopita ambapo haikuwa ikianza na kasi hiyo.

No comments:
Post a Comment