![]() |
| Moja ya timu ya kikapu nchini. |
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limehimiza timu
kuendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kombe
la Taifa yanayotarajiwa kuanza Novemba 11- 26 mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana Kamishna wa Ufundi na Uendeshaji wa
Mashindano wa TBF, Manase Zablon alisema timu nyingi zimekuwa na desturi
ya kufanya maandalizi mafupi matokeo yake zinapokutana ushindani
unakuwa mdogo.
Alisema timu zinatakiwa kujifunza kutokana na makosa kwa kuhakikisha maandalizi yao yanaanza sasa.
“Ili timu zifanye vizuri ni muhimu kwao kuanza maandalizi mapema,
kujiimarisha ili mashindano yanapofika kila timu ionyeshe ubora,
tunahitaji ushindani wa hali ya juu kupata washindi bora,” alisema.
Zablon alisema mashindano hayo yana umuhimu kwani ndiko sehemu
wachezaji wa timu za taifa huangaliwa na kuchaguliwa kwa kuwa hujumuisha
timu nyingi na zile za mikoani.
Hivi karibuni timu za Tanzania zilishindwa kufanya vizuri katika
mashindano ya Afrika Mashariki na Kati Kanda ya tano yaliyofanyika Dar
es Salaam, huku Zablon akisema sababu ni timu kushindwa kufanya
maandalizi ya kutosha ya muda mrefu.
Alisema timu zote zinahitaji kubadilika na kujifunza kutokana na makosa, kwa ajili ya kufanya vizuri wakati ujao.

No comments:
Post a Comment