Wednesday, October 12, 2016

TFF WAIKOMALIA YANGA YA KUKODISHWA.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesingwa.
Siku chache baada ya klabu ya Yanga kudai kuingia makubaliano ya kumkodisha klabu hiyo ya mitaa ya jangwani Mwenyekiti wao Yusufu Manji, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema halitambui mabadiliko ya uendeshwaji wa Klabu ya Yanga na wameuandikia uongozi wa Yanga barua wakitaka nakala ya mkataba wa ukodishwaji wa klabu hiyo kwa miaka kumi kwa mwekezaji anayetambulishwa kama Yanga Yetu.


Hayo yalizungumzwa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesingwa kwenye mkutano wake na waandishi na habari katika ofisi za Shirikisho hilo Karume, dar es Salaam hapo jana. Mwesingwa alisema, TFF imekuwa ikipokea barua kutoka kwa wadau mbalimbali wa Yanga wakihoji taratibu au hatua zinazoendelea katika mfumo wa umiliki na uendeshwaji wa timu hiyo. Siku chache zilizopita uongozi wa Yanga ulitoa taarifa kwamba Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo imeridhia kuikodisha kwa Kampuni ya Yanga Yetu kwa miaka kumi.

Uamuzi wa kukodisha klabu hiyo ulifikiwa na wanachama wa Yanga katika mkutano wa dharura ulioitishwa na Mwenyekiti wake Yusuf Manji Agosti mwaka huu, ambapo alisema ataikodisha nembo na klabu kisha baada ya miaka kumi atairudisha.
Alhamisi iliyopita vyombo mbalimbali vya habari vilikuwa na taarifa kuhusu muhtasari wa mkataba wa Yanga kukodishwa na Kampuni ya Yanga Yetu Limited.
“Simba na Yanga wamekuja na mabadiliko ya kutaka kubadili mfumo wa uendeshaji na tukaziandikia barua kutaka kukutana nazo kutaka kujua uhalisia na Simba walikubali, lakini Yanga Kaimu Katibu Mkuu wao (Deusdedit Baraka) alitujibu tuwasiliane na wajumbe wa Baraza la Udhamini ndiyo wenye majibu juu ya mchakato wa ukodishwaji,” alisema Mwesigwa.
“Baadaye tunasikia kwenye magazeti kuwa kuna kampuni moja ambayo wamesaini nayo mkataba... Ndipo tukashtuka hivyo tunataka kujua status (hadhi) ya mkataba. Je huo mkataba unahusu timu A tu na programu za vijana itakuwaje ndio vitu tunataka kujua japo klabu hiyo imesajiliwa kikatiba,” alisema Mwesigwa.
Kadhalika, Mwesigwa alisema wanataka kuona kilichopo kwenye mkataba kabla ya kushauri ili kuangalia kama kinakwenda sambamba na matakwa ya TFF, CAF na FIFA ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakiendelea kwani wengine wamefika hatua ya kuomba idhini ya TFF kwenda kumwona Rais John Magufuli.
Katibu huyo alisema wanataka kujua pia nani anamiliki na nani anaendesha timu na umiliki wake ukoje kwa maana timu za Simba na Yanga zinagusa nyoyo za watu wengi na taratibu za uhamishaji umiliki wake unatakiwa kuwa wa wazi-hadharani.
“Mambo ya kubadilishwa uendeshaji unatakiwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja kuenenda sawa na katiba ya klabu, kamati ya utendaji ifahamu, mkutano mkuu uridhie ili kujua nini kinauzwa na nini kinakodishwa ikiwa ni kwenye level (hatua) ya klabu. “Kama itakuwa nje ya utaratibu wetu wa uendeshaji wa klabu kamati ya sheria na kamati ya utendaji watafanya kazi na kama watakuwa wamefuata taratibu inaweza isifike huko kwenye CAF na FIFA,” alisisitiza Mwesigwa.
Mwesigwa alisema TFF itaendelea kuwasiliana na Kaimu Katibu Mkuu, Baraka au Mwenyekiti Manji kwa mambo yote yanayohusu sera na mipango na siyo bodi ya wadhamini kama ambavyo Baraka alielekeza.
Pia Mwesigwa alisema hawaangalii mtu anayekodisha ana fedha kiasi gani bali hata kampuni hiyo inatoka nchi gani na mmiliki ana historia gani huku amkimtolea mfano Roman Abromovich alipokwenda kununua Chelsea.
“Msimamo wa TFF ni kwamba Klabu ya Yanga ipo kama ilivyokuwa kwa mujibu wa taratibu za TFF, CAF na FIFA hadi hapo tutakapopata barua toka Yanga na tunatambua uongozi wa Mwenyekiti Yusuf Manji na Kaimu Katibu Mkuu Deusdedit Baraka,” alisema.
Alipoulizwa Kaimu Katibu wa Yanga Baraka alisisitiza kwamba suala hilo lipo kwa bodi ya wadhamini na ndiyo yenye uwezo wa kulizungumzia suala la ukodishwaji.

No comments:

Post a Comment