Thursday, October 13, 2016

TFF WAMTISHA MZIGO WA KESSY EL MAAMRY

Mwanasheria Mkongwe na mjumbe wa heshima wa CAF Said El Maamry.
Kufuatia klabu ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam kulikomalia Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) juu ya sakata la beki wao Hassan Kessy aliejiunga na mahasimu wao Yanga bila kufata utaratibu wa kisheria
Hali hiyo imepelekea TFF kumuandikia barua mwanasheria mkongwe na mjumbe wa heshima wa Shirikisho la soka Afrika (CAF), Said El Maamry kuweza kuamua juu ya sakata hilo lililopo baina ya vilabu hivyo viwili vikongwe nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Sheria na uanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Eliud Mvela aliiambia HabariLeo jana kuwa wamemuandikia El Maamry ili akutane na pande hizo mbili kumaliza suala hilo. Kikao hicho kati ya El Maamry na viongozi wa Simba na Yanga kinatarajiwa kukutana keshokutwa.

“Tumewasiliana na El Maamry na Jumamosi (keshokutwa) atakutana na Simba na Yanga ili kumaliza utata wa suala hilo, ikishindikana Kamati ya sheria na Hadhi ya Wachezaji itatoa maamuzi yake ambayo yapo ‘pending’,” alisema Mvela.

Alisema katika kikao cha mwisho Simba na Yanga walikubaliana kuwaomba mawakili Said El Maamry na Profesa Mgongo Fimbo kuwasimamia katika kikao cha kutafuta suluhisho la suala hilo.

Hata hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji chini ya Wakili Richard Sinamtwa ilikutana Septemba 24 iliwapa mahasimu hao siku tatu za kukaa na kumaliza suala hilo, hatua ambayo ilifikiwa baada ya mjadala mrefu kuhusu kesi mbili zilizofunguliwa na Simba mbele ya kamati hiyo.

Kesi hizo ni Yanga kudaiwa kuingia mkataba na Kessy wakati bado ana mkataba na Simba na ya pili ni mchezaji huyo kudaiwa kuanza kufanya mazoezi na timu hiyo pia kusajili Yanga na kwenda nje ya nchi wakati akiwa ndani ya mkataba klabu yake hiyo ya zamani.

Wakati inatoa agizo la kuzitaka klabu hizo zimalizane zenyewe, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilisema kama hawatafikia mwafaka, mashauri hayo yatarudi mbele ya kamati na kufanya uamuzi kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zinazoongoza mpira wa miguu Tanzania. Katika madai yake, Simba inataka ilipwe dola za Marekani 600,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.2).

No comments:

Post a Comment