Tuesday, October 11, 2016

VPL KUUNGURUMA KESHO, MBEYA CITY WAMTISHIA NYAU MNYAMA.

Kesho Jumatano Oktoba 12, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajiwa kuendelea kwa michezo saba kwenye viwanja tofauti na Mikoa tofauti nchini.

 Huku ule mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ukipangwa kufanyika Uwanja wa Uhuru baada ya klabu hiyo kuutambulisha Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani baada ya kupeleka maombi yao Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF), hilo linatokana na hatua iliyochukuliwa na Serikali ambaye ndiye mmiliki wa viwanja vya Uhuru na Taifa, kuzuia klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Simba kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa michezo yao ya nyumbani kutokana na vurugu zilizotokea baina ya timu hizo zilipocheza wikiendi iliyopita.

Huku mnyama Simba akiwa Mkoani Mbeya akicheza na Mbeya City ikiwa ni mara ya kwanza kwa Simba kucheza mechi ya nje ya mkoa wake. Huku wenyeji wao wakihakikisha kubakiza pointi tatu nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine. 
 
Kupitia msemaji wao wa timu ya Mbeya City, Dismas Ten alijitapa kwamba Simba wasitegemee kushinda kirahisi kama ilivyofanya kwenye mechi zake zilizopita kwani hata wao wamrjipanga na wanahitaji ushindi. Alisema wanaifahamu ni timu nzuri na wanaiheshimu , lakini ubora wao hauwaogopeshi katika kujituma na kupata ushindi.
“Simba wajiandae vya kutosha kwa sababu tumedhamiria kufunga magoli mengi, tunajua tabia zao wanapofungwa, lazima wakae,” alisema msemaji huyo.
 
Michezo mingine itakayopigwa Jumatano hii ni pamoja na ; Majimaji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
 
Stand United itaikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na katika mkoa huo huo Mwadui itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye dimba la Mwadui Complex huku timu pinzani za Mwanza ‘Mwanza Derby’ kati ya Mbao na Toto Africans itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo. 
Alhamisi Oktoba 13, 2016 Ruvu Shooting itacheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mabatini.

No comments:

Post a Comment