Wednesday, October 26, 2016

YANGA KUSHUKA DIMBANI KUMALIZIA KIPORO CHAO BILA HANS PLUIJM.


MABINGWA watetezi Tanzania Bara, Yanga watashuka dimbani leo kuwavaa JKT Ruvu katika mchezo wa kiporo, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru. Mchezo huo ulipaswa kuchezwa mwanzoni mwa msimu, lakini ilishindwa kufanya hivyo baada ya kusogezwa mbele kutokana na kukabiliwa na michuano ya kimataifa.

Kikosi hicho kitashuka dimbani bila Kocha wake Mkuu, Hans Pluijm aliyejiuzulu nafasi yake juzi, na sasa taarifa kutoka Yanga zinaeleza kuwa kikosi kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Juma Mwambusi na Meneja Hafidh Salehe hadi uongozi wa timu hiyo utakapoamua hatma yao.

Pluijm alijiuzulu baada kuwepo kwa taarifa za ujio wa Kocha mpya Mzambia wa Zesco George Lwandamina aliyekuwepo jijini kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Yusuf Manji, kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Pluijm. Mchezo huo ambao ni muhimu kwa Yanga kushinda ili wawaze kujitengenezea mazingira ya kuwa karibu na wapinzani wao Simba, ambao wamewaacha kwa tofauti ya pointi nane.
Yanga imeshacheza michezo 10, imeshinda sita, imepata sare tatu, na kupoteza moja ikivuna pointi 21 na JKT Ruvu imecheza michezo 11, imeshinda moja, ina sare sita na kupoteza minne ikishika nafasi ya pili kutoka mwisho kwa pointi tisa.

No comments:

Post a Comment