Mary Keitany raia wa kenya amekuwa mwanamke
wa kwanza kushinda mbio za Marathon za jiji la New York mara tatu
mtawalia katika kipindi cha miaka 30.
Keitany, 34, alitumia muda
wa saa mbili, dakika 24 na sekunde 26 na kuwa mwanamke wa kwanza kufanya
hivyo tangu raia wa Norway Grete Waitz - aliyeshinda mbio hizo mara
tano mtawalia.
"Kushinda mara tatu si rahisi, na ina maana kubwa sana kwangu. Si rahisi lakini nilifanikiwa," amesema.
Bingwa
wa dunia kutoka Eritrea Ghirmay Ghebreslassie, 20, alimshinda Mkenya
Lucas Rotich mbio za wanaume na kuwa mshindi wa Marathon ya New York
mwenye umri mdogo zaidi.
Ghebreslassie, aliyemaliza nambari nne
London Marathon na Olimpiki Rio alitumia muda wa 2:07:51 na kuwanyima
Wakenya ubingwa wa nne mtawalia katika Marathon kwa wanawake na wanaume.
"Najionea fahari sana kutokana na ushindi wangu, na kwamba mimi ni wa kwanza kutoka nchi yangu kushinda," amesema.
Mmarekani
Tatyana McFadden alishinda taji lake la nne mbio za wanawake wa kutumia
magurudumu New York akitumia muda wa saa moja dakika 47 na sekunde 43.
Sasa ameshinda mbio 17 kubwa za marathon zilizofanyika karibuni, zikiwemo London, Boston, Chicago na New York.
No comments:
Post a Comment